Vita: Kitabu cha Watoto

Imeandikwa na Zachary Gallant na Kutafsiriwa na Jason Isoe Maageria

Ni baada tu ya mlo wa jioni,
umeshiba na unahisi joto,
umekula ugali
na umemaliza kazi za nyumbani,
na kazi ya shule pia
na umemsaidia mama kuosha vyombo.
Baba na mama wameridhika.
Sasa ni wakati wa kupumzika
ni wakati wa kustarehe.
Mama anaiwasha televisheni
nawe unachukua vitu vya kuchezea kutoka chumbani.

Mama anapobadilisha stesheni
ili mtazame habari za jioni
Unaona mambo mengi
ambayo yanakuchanganya.
Wanataja mahali usikokujua,
kwenye majina ya kukanganya,
unaona watu wengi wanafuatana
na sura zao zinafanana.
Wote wanalia na kupiga mayowe,
nguo zao zimepakwa matope na uchafu;
wanapiga nduru, kuna huzuni,
akili yako inakuambia:
wote wanafanana.
Narudia tena:
wanafanana na wazazi wako,
sawa tu na rafiki zako,
sawa na dadako,
kakako, mwalimu wako,
sawa na mhubiri wako
au imamu au kasisi.

Ukionacho mahali huko usikokufahamu
ni kitu kiitwacho VITA.
Ni kitu ambacho watu wengi hupuuza.
Kwa sababu unahisi uko salama, nyumbani na mamako,
babako au nyanyako, paka wako na mbwa wako
unamkumbatia mwanasesere kwenye kitanda kizuri usiku,
baba ameshayafukuza mazimwi yote,
hakuna haja ya woga.
Ni rahisi kufikiri kila mtoto huishi hivi
lakini huu si ukweli katika dunia siku hizi.
Sehemu nyingi hazijabahatika kama sisi
uharibifu na huzuni ndio watu waonao tu.

Katika nchi za mbali
nchi zenye majina ya kutatanisha
watu wanaishi kwa woga;
wa majeshi na ndege,
ya maelfu ya mabuti,
mililipuko na mikuki.
Tu! tu! tu! ndio sauti ya bunduki
Wanapozifyatua.
Nyumba ya familia fulani,
walikoishi maisha yao yote
inaweza kuharibiwa kabisa
Katika usiku mmoja tu.

Ni rahisi sana kuogopa
na kuwalaumu wanaopigana
lakini mara nyingi huwa si makosa yao;
hata wao huwa wana uoga.
Wapiganaji wanaweza kufanya mambo mengi mabaya
lakini unapochunguza maisha yao,
utaona mambo yalipoanzia:
mara nyingi shida huwa kiwewe cha utotoni,
mtoto kama wewe anaibiwa kutoka kwa mamake.
Watoto wanaumizwa na dunia; utoto wao unajazwa na hasira.
Unaweza kutazama haya yakitendeka
Unapofungua kila ukurasa.

Wakati mwingine hasira zao huanza baadaye maishani,
labda kwa yule mjane aliyekuwa mke wa fulani.
Wakati mwingine inafanyika kwa msururu wa miaka kadhaa,
televisheni na serikali inapowatisha jamaa.
Inatendeka pole pole, wala si mara moja tu,
Nchi yote inaweza kushawishiwa kuua
kwa sababu ya jambo la kipumbavu kama umiliki wa kilima chenye maua,
au bendera, kitambaa tu chenye rangi tatu,
au kabila, au rangi ya ngozi, au jina la mtu.

Je wataka kujua ni kwa nini ni rahisi kukuza chuki?
Ifikirie historia ya familia yako:
kama babu angekueleza kuhusu wauaji
katika kijiji jirani
waliochukua shamba la babu yake,
Akakueleza kuhusu jamaa wenu waliouawa.
Je, unafikiri ungefurahia?
Kama ungeenda huko uone hilo shamba
na upate msichana mwenye rika lako na tabasamu usoni
hungefikiri kama wengi wanavyofikiri?
kwamba familia yake yote ina hatia,
huyo msichana mdogo pia?
Utakumbuka, kama mtoto mwenye busara,
kwamba huyu mtoto sio kama wazazi wake walioleta hasara.
Chochote kilichofanyika karne moja au mbili zilizopita,
msichana huyu mdogo kama wewe hakuwa wakati wa vita.

Kuna watu ambao
fikira zao ni tofauti na zako,

ambao watawalaumu watoto
kwa makosa ya wengine.
Wanaamini kwamba huyo msichana anafaa kulaumiwa
kwa sababu ya mikosi na uchungu waliopitia.
wanafikiri kila kilichowafanyikia
kila kilicho kibaya maishani mwao
kingekuwa vizuri wakilipiza kisasi kwa huyo msichana.
Na, uhalifu wanaoukumbuka
ni wa zamani za kale,
sio ya babu za babu zao, ila karne na karne zilizopita.
Na mji anapotoka huyo msichana wana maoni tofauti:
eti kwamba babu yako alitenda mabaya na wewe pia ni mbaya.
Miaka mingi imepita
tangu kuwe na hivyo vita,
lakini kila mahali kuna hadithi za kutisha
hadithi za mji huo mwingine ambao sasa una amani.
Wanawatisha watoto wao na kuwapa mafunzo ya vita jangwani
na mvutano unaongezeka, ‘hatimaye usiku mmoja,
miji hiyo miwili inapigana- Naam wote wanachangia pamoja,
hadi mtu afe jamii ipoteze mwangaza,
hivyo ndivyo vita nyingi huanza.

Fikiria kuhusu habari ambayo mama alitazama kwenye runinga:
Je, ni nani anayechagua kuonyesha mnachokitazama kwenye runinga?
kampuni za habari zinapata pesa nyingi watu wanapotazama habari
na habari za kutisha huwafanya watu wengi kutazama.
Vita ni biashara kwa runinga na magazeti
kwa hivyo wakati mwingine wanabuni habari.
Picha za watu wenye hasira zinaonyeshwa,
kisha habari za kuogofya zinatangazwa kuwafanya kuogopa.
Wanakuelezeni kuwa watu hao wanawachukia
lakini hawawaelezi sababu.
Wanahabari wanawaita maadui wanaotaka kuona tumekufa kama mababu.
Na tunaamini kwamba wanahabari hawawezi kutudanganya,
lakini kila hadithi ina pande mbili.

Ukiamini kinachoonyeshwa kwenye runinga
baada ya miezi kadhaa ya kutazama,
watageuka kuwa adui zako.
Lakini watu hao ambao habari imekueleza kuwa ni wajeuri
wanaweza kuwa wazazi wa mtoto mzuri.
Wanaongea lugha tofauti
na wanasema maombi tofauti,
lakini wanaweza kuwa na sababu halisi
kukunja ngumi tayari kupigana.
Labda wanachukia nchi yako,
lakini hawakuchikii wewe binafsi.
Mara nyingi huwa wana hasira
kwa sababu ya vile serikali inafanya mambo.

Labda nchi yako ilimuumiza mtu mzuri
na sasa wana uchungu,
Kama babako anavyoweza kufanya.
Ingeweza kuwa rahisi kurekebisha kama tungewaelewa
na wao vile vile watuelewe,
si wangeshangazwa
Jinsi ulivyo mzuri! Mzuri tu kama mtoto wao!
Vita ingeepukika kama tungeelewana nao.

Hii si kusema kwamba huwezi kujihusisha,
kugombana wakati mwingine si hatia.
wakati mwingine watu hupigana
nyumbani kwenu mnaweza kupigania haki
baada ya uongozi mbaya,
Waingereza wameipa hali hiyo jina, jina lenyewe “Springi”
ni ambapo watu wanainuka na kupinga mateso
kutokana na uongozi wa madikteta wanaowatesa na kuwaua watu kwa sababu wana uwezo.
Lakini hii si vita, huku ni kupigania uhuru wa watu.
Tofauti ziko, ukifungua macho na kutazama kwa jicho la tatu.
Watu wanapogigania uhuru wao,
kuongea, kupenda, kuomba,au kutulia
viongozi wao, watu wenye silaha
wanawaumiza wananchi wasio na silaha,
kwa sababu uongozi wao unatikiswa.
Na wakati mwingine wananchi wanaoteseka wanahitaji usaidizi
wanapokosa nguvu ya kujipigania.
Wakati kama huu, hawana budi kupigana na kuumia,
lakini ni vigumu sana kujua wenye hatia na wasio na hatia.

Sababu, au sehemu inapoanzia haijalishi,
vita ni kitu kinachotuletea mazishi.
Wasichana wanawapoteza baba na wavulana wanawapoteza mama zao
na wazazi wanawapoteza watoto pale mabomu yanaposimama,
kukiwa na risasi, na malori ya kijeshi,
kukiwa na majeshi yanayofuata amri tu
bila kujua hatima ya vitendo vyao
wametumwa na serikali kupigania mchanga wao.

vyanzo vya shida hizi vimeandikwa wazi kwenye ubao,
ni neno tunalolitumia, neno lenyewe ni “wao”.
Tunajiuliza maswali kama
“Ni nini mbaya na watu wale, jameni hawana haya?”
Ni fikira ndogo kama hiyo ndiyo chanzo cha mabaya.
“Wao” na “watu wale” ni binadamu nakuambia
wenye mapua ya kupumulia na macho ya kutazamia,
wenye akili zenye kufikiria mawazo mema
Kama yako tu inayopenda wema.
Unaweza kumzubalia mtu
aliyevaa mavazi yaliyochanika tu
mwenye rangi tofauti au pua ndefu.
Huyu mtu ni wa kipekee, ni mgeni.
Usijiulize, ni nini hicho?
Badala yake jiulize, “wewe ni nani?”
kwa sababu unachokifikiria ndicho,
anachokifikiria pia anapogeuka kukuangalia,
mtu huyu mgeni labda anafikiri hivyo pia.
Ni rahisi sana kuanguka kwenye mtego huu
mtego wa kutengana bila sababu.
Kwa hivyo jaribu kukumbuka
mawazo maovu yakikuibuka
kuhusu watu watokao sehemu tofauti na sisi
au rangi au alama ya kuzaliwa
kwamba nawe pia si tofauti sana
ukilinganishwa na wale watoto waliokumbwa na vita,
ni kwa bahati tu wewe ulizaliwa ambako vita haikupita.
kokote uendako, chochote ufanyacho,
dunia hii yote ina watu kama wewe.
Imejazwa nami,
imejazwa nasi, ni yetu sote.
Tunapowaruhusu watu kututenganisha kwetu
tunapoteza mazuri yote yaliyo ndani yetu.

Nchi zinazouza tarakilishi na magari mengi
zinazosaidiana kuwatuma watu wao kwenye mwezi
ukifuatilia vizuri waliwahi kupigana vita kubwa kwenye historia
sababu halisi za vita haijui Musa wala Maria,
kusababisha chuki vinywani
au sura zao hadi ziwafike kooni
ya watu kuwaua wenzao kwa hasira na chuki,
mpaka mmoja aseme “tulieni!”
Ndipo kunapokuwa na afueni.
Kisha inakuwa ni kama hakuna kilichotendeka, au watu wanajifanya kusahau
Kupuulizia miaka mingi amabayo watu walipigana
kana kwamba walikuwa marafiki,
Wanatuacha bure tu waliokufa kwa mikuki.
Kulikuwa na njia kadhaa,
kama wataalamu wangehusishwa.
Sasa tumewapoteza mamilioni ya wapendwa
ambao wangekuwa rafiki zetu
kwa sababu viongozi wavivu
waliamua kupigana, badala ya kujadiliana.
Na kati ya hao mamilioni
kulikua na nyota iliyowaka
mwangaza ambao ungeleta matumaini
na furaha nyingi duniani.

Haya ni maelezo ya vita,
mizizi yake na chanzo chake.
Vita ilikuwa hata kwa vizazi vilivyopita,
Kukiwa na hali tulivu katikati.
Tofauti leo ni vile tunavyoifikiria.
Watu walifikiri kuwa vita ilikuwa kitu kizuri,
kama waweza kuamini,
lakini vita imeleta uchungu mwingi,
suluhisho la kivivu ambalo halihitaji kufikiria sana.
Vita ni tatizo, si jibu.
Kupigana ili kutatua shida kunachipua jipu.
Ukitazama haya yote, yanaweza kukufika kwenye koo,
lakini hakuna kitakachobadilika tukisema “ndivyo ilivyo!”
hisia za kukosa imani, kuwa na shaka, au kukata tamaa:
Tunaweza kumaliza vita, kama sote tungejadiliana.

Sasa unajiuliza maswali mengi kama, nitasaidiaje?
Kumbuka kunaweza kuwa na amani duniani,
na amani inaanza nawe jamani.
unaweza kuonyesha mapenzi, na kuwa mzuri pia
kila mtu, hata wanaokutendea mabaya.
Usiwaruhusu wakulazimishie chochote,
lakini jaribu kuwaelewa:
ni nini kiwafanyacho watende mabaya,
ni nini kiwafanyacho wawe na uchungu mwingi?
Kama hutopigana
na badala yake
ujaribu kuondoa uchungu mioyoni mwao
bendera hufuata upepo wanaweza kufuata ukarimu wako.
Kama tungetazama kupitia kwa macho ya wenzetu,
vita ingeisha, hakuna haja ya watu kuendelea kufa.

Na haya yote, haya yote, yote yanaanza na wewe.
Una nguvu nyingi kushinda unavyofikiria.
Inaanza nawe, na nguvu za mapenzi tele
tunaweza kukomesha kutupa mabomu ya kuua,
na badala yake tuanze kutuma maua.

 

Advertisements